BBC Kusaka wafanyabiashara vijana


BBC inatafuta vijana wenye mawazo ya kibiashara kushiriki katika shindano lijulikanalo kama Faidika na BBC, litakalozinduliwa rasmi Jumatatu Aprili 21 2008.

Faidika na BBC inaalika vijana wanaozungumza Kiswahili, na wenye umri wa kati ya miaka 16 hadi 24, kuwasilisha michanganuo yao, ya jinsi ya kuanzisha biashara ambayo itanufaisha jamii. Mchanganuo huo utatakiwa kuwiana na bajeti ya Dola za Marekani 5,000, zitakazotolewa, ikiwa ni zawadi ya kwanza na kuwa msingi wa biashara hiyo. Mchanganuo usizidi maneno 1,500. Michanganuo itumwe kwa: faidika na BBC, PPF Building, 8th Floor, P.O Box 79545, Dar es Salaam. Au kwa barua pepe: faidika@bbc.co.uk.

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Solomon Mugera, amesema "Shindano hili ni fursa kwa vijana wenye kuona mbali, na ni nafasi yao ya kutimiza ndoto zao. Hii pia ni nafasi kwa vijana kujisaidia wao wenyewe na jamii zao kwa ujumla".

Salim Kikeke, Meneja Mradi wa Faidika na BBC ameongeza "Nina imani kuwa vijana wengi wana mawazo mazuri na ya kuvutia ya kibiashara. Kwa wale ambao hawatashinda zawadi ya kwanza, tutajitahidi kuwatafutia ushauri wa kuwasaidia katika kutimiza ndoto zao".

Kutakuwa na mchuano wa kutafuta mshindi mmoja kutoka kila nchi. Kuna jumla ya nchi sita zinazoshiriki katika shindano hili. Nchi hizo ni Burundi, Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Mchuano wa kutafuta mshindi wa Rwanda na DRC utafanyika kwa siku moja. Mchuano wa Tanzania utafanyika Jumatano tarehe 4 mwezi Juni. Mshindi kutoka nchi husika atazawadiwa cheti maalum na kombe.

Washindi sita, mmoja kutoka kila nchi zilizoshiriki, watapambana kuwania nafasi ya kwanza mjini Kampala, Uganda, Jumatano, tarehe 18 Juni. Fainali hiyo itatangazwa moja kwa moja kupitia matangazo ya jioni ya BBC, Dira ya Dunia, na vilevile katika mtandao kupitia bbcswahili.com. Mshindi atapata dola elfu tano za Marekani, pamoja na Kombe. Jopo la majaji litaundwa na wafanyabiashara vijana kutoka Afrika Mashariki na Kati.

David Ssegawa, kijana mwenye umri wa miaka 22, raia wa Uganda, alikuwa mshindi wa Faidika na BBC mwaka jana baada ya kuwashinda washiriki wengine zaidi ya 5,000, kutoka eneo la Afrika Mashariki na kati, wanaozungumza Kiswahili. David aliandika mchanganuo wa utengenezaji mishumaa. Hivi sasa amekwisha anza biashara yake na inaendelea vizuri. Kupata habari zaidi kuhusu David Ssegawa, pamoja na shidano la Faidika na BBC ingia katika mtandao wetu bbcswahili.com.

0 Response to "BBC Kusaka wafanyabiashara vijana"

Powered by Blogger