Magari ya Rais yazima tena safarini!!!

UDANGANYIFU unaofanywa wa kuchanganya petroli na mafuta mengine jana uliyakumba magari matatu yaliyotakiwa kuwa kwenye msafara wa rais ambayo yalipata hitilafu na kulazimika kutoendelea na safari kutokana na kuwekewa mafuta hayo.Tukio hilo limetokea siku chache baada ya gari alilokuwa amepanda Rais Jakaya Kikwete kupata tatizo la tairi ambalo lilichomoka muda mfupi baada ya mkuu huyo wa nchi kuhamishiwa gari jingine wakati akiwa kwenye ziara ya siku moja jijini Dar es salaam.

Bughudha hizo ziliendelea kuifuata Ikulu jana baada ya tukio hilo kutokea majira ya saa 4:30 asubuhi mjini Moshi na kuwa gumzo kubwa kwa wakazi wa hapa. Magari hayo yaliweka mafuta kwenye kituo cha Total kinachomilikiwa na mfanyabiashara Epimark Laswai na kusababisha hitilafu hiyo iliyozuia magari hayo kuendelea na msafara.

Magari hayo ya ulinzi yaliyowekewa mafuta kwa ajili ya kujiandaa kwenda Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kumpokea Rais Jakaya Kikwete, ambaye alitarajiwa kuwasili saa 11:40 jioni.

Habari za uhakika zilizothibitishwa na maofisa wa vyombo vya dola ziliidokeza Mwananchi kuwa kituo hicho kimewekwa chini ya ulinzi wa polisi na maofisa Usalama wa Taifa na watu watatu wanashikiliwa na polisi.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, mara baada ya magari hayo aina ya Toyota VX V8 rangi nyeusi kuweka mafuta, kifaa maalumu (sensor) ndani ya magari hayo kilibaini kuwa mafuta hayo hayana ubora unaokubalika.

Jitihada za maofisa usalama kuyawasha magari hayo zilishindikana hadi mafundi wa kampuni ya Rajinder Motors walipoitwa na kumwaga mafuta yote yaliyokuwa yamewekwa katika magari hayo.

Habari zaidi zimedai kuwa kituo hicho kimewekwa chini ya uangalizi wa polisi na maofisa usalama hadi wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) watakapochunguza ubora wa mafuta hayo.

“Tayari wataalamu wa Ewura wako njiani kuja Moshi kwa ajili ya kuchunguza kituo hicho kama kulikuwa na hujuma kwa msafara wa Rais Kikwete au ni hujuma za uchanganyaji wa mafuta,” kilidokeza chanzo kimoja cha habari.

Mmiliki wa kituo hicho, Epimark Laswai alithibitishia Mwananchi kuhusu tukio hilo na kufafanua kuwa jana asubuhi kituo chake kiliishiwa mafuta na kulazimika kununua mafuta ya dharura kutoka kituo kimoja jijini Arusha.

“Wafanyakazi wangu waliwasiliana na Mount Meru Arusha ambao walituletea lita 4,000 na tulipoyamwaga tu kwenye visima vyetu ndio hayo magari ya Ikulu yakaja yakaweka mafuta na ndio matatizo yote yalipoanzia,” alisema.

Laswai alisema alifanya jitihada kutafuta mafuta mengine masafi ambayo yanaoana na magari hayo na kuhakikisha wafanyakazi wote watatu wa Mount Meru walioshiriki kuleta mafuta hayo, wanawekwa chini ya ulinzi wa polisi.

Mfanyabiashara huyo alisema hata lori lililobeba mafuta hayo limewekwa chini ya ulinzi wa polisi.

0 Response to "Magari ya Rais yazima tena safarini!!!"

Powered by Blogger