Utapeli wa aina mpya Dar

*Matapeli wajifanya waganga wa jadi
*Mwanajeshi mstaafu ajikuta akiuza nyumba, gari
* Alirubuniwa anatafutiwa tiba ya tumbo

UTAPELI wa aina yake umeibuka jijini Dar es Salaam na kusababisha watu mbalimbali kujikuta wakipoteza mali zao katika mikono ya matapeli wanaosadikiwa kutumia nguvu za giza kuwarubuni watu.

Katika sakata la hivi karibuni, mzee aliyefahamika kwa jina la Said Makau, mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amejikuta akiuza mali zake zote ikiwamo nyumba, gari na vitu vya ndani vyenye thamani ya zaidi ya Sh 71.5 milioni bila kujijua.

Tukio hilo lilitokea katika eneo la Bonyokwa Vyumba Vinane jijini hapa baada ya Makau kudaiwa kuwa alikuwa akidanganywa na matapeli kwa kunyweshwa dawa za kienyeji ili kumzubaisha akili.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake, Makau, alisema watu hao walimwandama kwa takriban mwaka mzima ambapo awali yeye na familia yake walikuwa wakiishi katika eneo la Tandale kabla ya kuhamia katika nyumba yao, Septemba mwaka juzi katika eneo hilo la Kimara.

Alisema mara nyingi amekuwa akisumbuliwa na tumbo la kujaa gesi, jambo lililomfanya ahangaike katika hospitali nyingi bila mafanikio na ndipo alipokutana na kijana mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye ni fundi simu.

Alisema baada ya kumhadithia kijana huyo matatizo yake, alikubali kumsaidia kwa kumwambia kuwa yanaweza kutatuliwa na waganga wa jadi ambao anawajua.

Mwanajeshi huyo mstaafu, alisema kijana huyo tangu hapo amekuwa karibu na familia yake na kwamba baadaye hakuweza hata kushtuka kuwa anaweza kumgeuka.

Alisema siku ya siku bila kujua kuwa anatumbukizwa katika dimbwi la kitapeli, alikubaliana na kijana huyo kwenda kwa mganga eneo la Kibangu na kuwakuta vijana wengine ambao walijitambulisha kuwa ndio waganga wa jadi.

Alisema watu hao walimweleza kuwa ni kweli ana matatizo makubwa kwani nyota yake imechafuka na kama hatapatiwa dawa kwa haraka angeweza kupoteza maisha yake kwa kifo cha ajali na familia yake yote ingeteketea.

Kwa mujibu wa Makau, walimpatia dawa za kunywa zilizowekwa katika glasi ya maji na hirizi ambazo alidai ndizo zilisababisha kuchanganyikiwa na kuwa katika hali ya kupoteza kumbukumbu, kisha kukubali kufanya kila jambo analoamrishwa bila kukataa ama kujua kama ni baya ama zuri.

Alisema kabla ya kunywa dawa hiyo, waganga hao walimpa masharti atumie peke yake bila kumshirikisha mkewe na kumuonya akimwambia mtu atakufa pamoja na watoto wake wote.

Alisema siku zilizofuata kijana huyo akiwa na mwenzake walimfuata nyumbani kwake na kumweleza kuwa, anatakiwa kutoa kadi za gari na gari lake aina ya Hiace alilokuwa akilitumia kama daladala kwa safari za Ubungo- Segerea ili litambikiwe kwa mizimu.

Akielezea jinsi utapeli ulivyofanyika, mzee huyo, alisema matapeli hao walimfuata na kumwambia kuwa kama hatalipeleka gari lake kwenye mizimu kuombewa litaweza kuua watu wengi ndani ya wiki moja; na kumsababishia matatizo makubwa kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani na kutiwa hatiani.

Ili kuendelea kudumisha miiko ya waganga wale, alisema ilimlazimu kumdanganya mkewe na watoto wake kuwa gari linapelekwa kutengenezwa.

Alisema walimwelekeza kulipeleka gari hilo na kadi zake katika maeneo ya Manzese kwenye ofisi iliyoko uchochoro wa Moshi Hotel na kuwakabidhi.

Makau anasimulia kuwa, alipowakabidhi, walilizunguka gari hilo kana kwamba wanaliagua kisha kumwambia inabidi liuzwe ili anunuliwe jingine kulingana na mizimu ilivyoamua.

"Niliposita watu wale waliniambia basi itabidi niliache gari langu pale ili waendelee kuliagua na wakaniomba nirudi kulifuata baada ya wiki moja kazi ya maombezi itakuwa imekamilika," alisema.

Katika kumwondoa hofu, alisema watu wale walimwambia asaini kwenye mkataba wa makabidhiano, ili akija kulichukua kusiwe na hadithi yoyote.

Kwa kuhofia madhara yanayoweza kutokea kwa kusababishwa na gari hilo, alikubali kuliacha gari hilo huku akiwa hana majibu kwa nini alikubali kufanya hivyo.

Baada ya wiki kupita, alikwenda kwenye ofisi ile kuchukua gari lake, lakini alistaajabu baada ya kukuta haipo wala watu hawapo. " Nilipoona sielewi niliamua kuuliza baadhi ya watu maeneo yale ambao hawakuwa wakinielewa natafuta nini," alisema.

Aliamua kwenda kituo cha polisi kutoa taarifa na kupewa RB kwa ajili ya kuwakamata watuhumiwa hao.

�Njiani nikakutana na yule bwana aliyejifanya kama karani siku ile nikamsimamisha nikataka kumuuliza inakuaje, aliponiona alikimbia mbio na kuniacha nikiwa na butwaa,� alisema.

Alisema alipoona siku zinakwenda aliamua kumtafuta yule kijana ili amweleze kuwa watu wake wamemtapeli, akamtuliza asiwe na wasiwasi kwa kuwa gari wameliuza na watamnunulia jingine.

"Walipoona kuna dalili za njama zao kujulikana waliniletea dawa nyingine na kumshauri kutumia tena, ila safari hii ampe na mke wake na nyingine wapigie deki nyumba yote ili apone haraka na waendelee kutunza siri yao," alisema

Makau, alisema dawa hizo ziliendelea kumchanganya na mkewe, na kwamba kwa safari hiyo, walikuwa na mkakati wa kumtapeli nyumba na kuchukua vitu vyote vya ndani vyenye thamani ya Sh 1.5 milioni kwa madai kuwa wanaenda kuvipooza kwa mdawa.

Alisema walipovichukua vitu hivyo walienda kuviuza kwa Sh 450,000 kisha kurudi kumchukua yeye na kumpeleka katika makaburi ya Ismailia yaliyopo Makumbusho, ambako walimsomea dua kwa saa mbili wakidai kuwa angepata nafuu.

Alisema katika hali isiyo ya kawaida, siku tatu zilipopita tangu wachukue samani hizo, walirudi tena nyumbani kwake na kudai kuwa nyumba wanayoishi ina majini mengi, hivyo ni vema wakaiuza na kununua nyingine, kabla hayajaanza kuwadhuru.

Baadaye kijana huyo akiwa na mtendaji serikali za mitaa, Athuman Mtono, walifika nyumbani kwake na kumweleza kuwa anatakiwa kuita mashahidi kwani wateja wa kununua nyumba tayari wamefika.

Alilazimishwa kusaini fomu iliyoandikwa hati ya uthibitisho wa kiwanja badala ya hati ya mauzo ya nyumba bila kujijua kuwa ndiyo anauza nyumba kwa mnunuzi kwa gharama ya Sh22 milioni.

Baada ya kusaini hati hiyo, mdogo wake mnunuzi wa nyumba hiyo alitoa Sh 1milioni na kudai fedha nyingine kiasi cha Sh 21 milioni zitapelekwa kesho yake na kwamba ananunua kwa ajili ya kaka yake ambaye hakuwepo siku ya tukio hilo.

Mtono lithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa Makau aliamua kuuza nyumba yake kwa ridhaa yake mwenyewe kwani siku ya tukio alikuwapo mkewe na mtoto wao.

Naye Mjumbe wa Shina, Raphael Fikiri alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa walikabidhiwa fedha kiasi cha Sh20,000 kila mmoja kama mashahidi wa kuuzwa kwa nyumba hiyo.

Fikiri, alisema baada ya tukio la kuuzwa kwa nyumba hiyo, alishuhudia teksi ikifika katika eneo la nyumba na kuondoka na mtuhumiwa.

Makau, alisema waligundua kuwa wametapeliwa wakati mnunuzi alipokwenda kuwatoa katika nyumba yao na ndipo walipochukua hatua ya kwenda kuripoti katika Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusufu na kupewa RB/749/2008 ili watuhumiwa waweze kukamatwa.

Alisema kwa kushirikiana na askari wapelelezi walifanikiwa kumkamata kijana huyo, eneo la Malamba akiwa anasimamia ujenzi wa nyumba yake.

Baada ya kukamatwa wameendelea kufuatilia kesi hiyo maeneo mbalimbali ya usalama, lakini amekuwa akizungushwa, wakati huo huo wanunuzi wa nyumba hiyo wanawashurutisha kuhama kupitia kwa mtendaji.

Alisema hivi sasa wamepewa barua yenye kumbukumbu namba MAA/DL-03/08/11 kutoka kwa wakili wa wanunuzi hao, ambao ni kampuni ya (M&A Advocates ) inayowataarifu kuwa wanatakiwa kuhama, vinginevyo hatua za kisheria zitafuata.

Mwananchi ilifanikiwa kuongea na mpelelezi wa kesi hiyo kutoka katika Kituo cha Polisi cha Mbezi kwa Yusufu ambaye alikiri tukio hilo kuripotiwa kituoni hapo.

Hata hiivyo, alikataa kuzungumzia zaidi kwa madai si mzungumzaji wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kinondoni bali, mwenye dhamana hiyo ni Kamanda Jamal Rwambo.

Habari za ndani kutoka polisi zinadai kuwa jalada lililokuwa na vielelezo vya kesi hiyo vilibadilishwa ili kuweza kumtetea mtuhumiwa asiweze kukabiliwa na kesi ngumu ya kitapeli dhidi ya Makau.

Inadaiwa kuwa kutokana na ubabaishaji katika kesi hiyo, mpelelezi mkuu wa kanda alimwamuru askari huyo, kupitia upya mwenendo wa kesi hiyo ili mambo yote yaweze kutendeka kwa haki.

Kamanda Rwambo alipohojiwa kwa simu na Mwananchi alisema kuwa ni vema akapewa muda ili aweze kufuatilia jambo hilo, kwani tukio hilo lilipotokea alikuwa yuko likizo, hivyo asingeweza kuongea kitu chochote.

Hata hivyo, katika uchunguzi wa polisi na familia ya Makau, gari hilo limekamatwa na linadaiwa kuuzwa kwa watu wengine wawili na baadhi ya vitu vimerudishwa baada ya Mzee Makau kutumia fedha kuvikomboa kutoka katika mikono ya waliovinunua.

0 Response to "Utapeli wa aina mpya Dar"

Powered by Blogger