Adaiwa kufa kwa kunywa ‘Viagra’!!!

Na gazeti la mwananchi.

MJI wa Arusha mwishoni mwa wiki ulizizima baada ya kutokea habari za kifo cha kutatanisha cha mkazi wa Levolosi, Omari Salim, 44, aliyefariki dunia wakati akipelekwa Hosptali ya Mt Meru baada ya kuzidiwa akiwa nyumba ya wageni na mpenzi wake.

Tayari Jeshi la Polisi mjini hapa limeshathibitisha kutokea kwa tukio hilo, lililoibua maswali mengi kwa wakazi wa mjini hapa. Polisi imedai uchunguzi wa awali umebaini kifo cha marehemu huyo kimetokana na utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu za kiume.

Polisi imezitaja dawa hizo kuwa ni aina ya Muco zilizokutwa ndani ya chumba alichokodi kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni.

Kaimu kamanda wa polisi mkoani hapa, Akili Mpwapwa aliiambia Mwananchi kuwa Mei 26 majira ya saa 8;30 Salim alimpigia simu mpenzi wake aliyetambulika kwa jina la Caren Isaack, 20, ili wakutane. Alisema wote kwa pamoja walikubaliana na kwenda kukodi chumba katika nyumba ya kulala wageni ya Rhino.

Alisema baada ya wapenzi hao kuwasili ndani ya chumba hicho, mpenzi wake alimwambia Salim kuwa wapande kitandani kwa lengo la kufanya mapenzi, lakini marehemu alilalamika kuwa alikuwa akijisikia vibaya na ndipo alipoomba kwenda bafuni kuoga.

Kwa mujibu wa Mpwapwa, marehemu aliingia bafuni kuoga, lakini ghafla alitoka akiwa ameshika taulo mkononi huku akitetemeka, ndipo mpenzi wake alipopatwa na mshangao.

Alidai kuwa kadiri muda ulivyokuwa ukienda, ndivyo hali ya Salim ilivyozidi kubadilika na ndipo akaamua kumbeba na kumweka kitandani na baadaye kumfunika shuka, lakini ghafla akaanza kutapika mfululizo.

Kamanda Mpwapwa alifafanua ya kuwa Caren alilazimika kuomba msaada kwa mlinzi wa siku hiyo ndipo walipofanikiwa kumtoa chumbani na kukodi teksi kumuwahisha hospitalini, lakini akakata roho wakiwa wakiwa njiani.

Alidai ya kuwa jeshi la polisi lilikuta vidonge mbalimbali vya dawa zinazosadikiwa kuwa ni za kuongeza nguvu za kiume zilizokuwa katika pakiti na kwamba huenda Salim alimeza vidonge hivyo kabla ya kushiriki ngono.

Kamanda Mpwapwa alisema polisi wanamshikilia Caren kwa uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo

0 Response to "Adaiwa kufa kwa kunywa ‘Viagra’!!!"

Powered by Blogger